London, England
Kocha wa Burnley, Vincent Kompany (pichani) amesema timu hiyo haiogopi kitu kwenye Ligi Kuu England (EPL) baada ya kufuzu kucheza ligi hiyo msimu ujao ikiwa imebakiwa na mechi saba.
Ushindi wa mabao 2-1 ambao timu hiyo iliupata jana Ijumaa dhidi ya Middlesbrough kwenye Championship ulitosha kuifanya irudi kwa mara nyingine kwenye EPL ambayo ni ligi kubwa ya soka England.
“Hatuhitaji kuwa tayari kwa sasa, ndio kwanza tuko Aprili kwa hiyo tuna miezi mingine mitatu ya kuhakikisha kila kitu kinakuwa tayari,” alisema Kompany.
”Kwa hakika nina furaha tele kwa klabu hii na kwa kila mtu aliyehusika, hili ni jambo la kipekee, bado nina kila sababu ya kusema kwamba tukio kubwa zaidi litakuwa tutakapobeba taji jambo ambalo kwa sasa bado hatujalifikia,” alisema Kompany.
Burnley ilishuka daraja msimu uliopita baada ya kucheza EPL kwa misimu sita ambapo baada ya kushuka baadhi ya wachezaji muhimu waliachana na timu hiyo.
Kwa msimu huu hadi kupanda daraja, Burnley imeshinda jumla ya mechi 25 za Championship na kupoteza mbili tu katika mechi 39 hadi kuhitimisha msimu.
Mwenyekiti wa Burnley, Alan Pace alisema kwamba timu yao kufuzu kucheza EPL ni jambo la kushangaza na ambalo hawakulitarajia.
“Hili halikuwa katika mipango yetu, mimi na Vincent tulijadili hili wakati wa majira ya kiangazi na tukajipa miaka miwili hadi mitatu, kilichotokea ni maajabu,” alisema Pace.