Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Azam, Dani Cadena ametamba kuipa timu hiyo Kombe la FA (ASFC) msimu huu baada ya kuona mbio za kulitwaa taji la Ligi Kuu NBC zimekuwa ngumu.
Azam imepangwa kucheza na Mapinduzi FC, katika hatua ya 16 bora ya michuano hiyo ambayo mechi zake zinachezwa mfululizo wiki hii.
Akizungumzia maandalizi yao kuelekea mchezo huo, kocha huyo ameeleza kuwa yeye na wachezaji wake wamekubaliana kubeba taji hilo ikiwa ni ishara ya kuwapoza viongozi na mashabiki wao ambao walikuwa na matarajio makubwa na ubingwa wa ligi kuu msimu huu.
“Akili na nguvu kubwa kwa sasa tumeziweka kwenye Kombe la FA, lengo ni kuwapoza machungu waliyokuwa nayo mashabiki wetu kwa kukosa ubingwa wa Ligi Kuu ambapo mpaka sasa kumesalia mechi chache,” alisema Cadena.
Kocha huyo raia wa Hispania ameeleza kuwa kitu kinachompa nguvu ni utayari ambao wachezaji wake wanamuonesha mazoezini na kitu kizuri kwake hakuna mchezaji majeruhi kwenye kikosi mpaka sasa.
Alisema pamoja na kutowajua vizuri wapinzani wao Mapinduzi lakini hawatowadharau sababu anachoamini ni timu nzuri ndio maana imefika hatua hiyo.
Rekodi zinaonesha kuwa Azam imebeba taji hilo mara mbili tangu kuanzishwa kwa michuano hiyo ya Kombe la FA, ambapo bingwa wake anaiwakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.