Rabat, Morocco
Real Madrid jana Jumamosi ilibeba taji la klabu la dunia la mwaka 2022 baada ya kuinyuka Al-Hilal ya Saudi Arabia mabao 5-3 na kuweka rekodi ya kubeba taji hilo kwa mara ya tano.
Katika mechi hiyo ya fainali iliyopigwa mjini Rabat, Morocco, Real Madrid ambao pia ndio mabingwa wa Ulaya, waliandika bao la kwanza dakika ya 13 lililofungwa na Vinicius Junior akiitumia pasi ya Karim Benzema.
Dakika tano baadaye Madrid waliandika bao la pili mfungaji akiwa Valverde lakini Moussa Marega aliibua matumaini ya Hilal alipoipatia timu hiyo bao la kwanza kwa pasi ya Kano na timu kwenda mapumziko Madrid wakiwa mbele kwa mabao 2-1.
Madrid ilikianza kwa kasi kipindi cha pili na dakika 10 tangu kuanza kipindi hicho iliandika bao la tatu lililofungwa na Karim Benzema aliyeinasa pasi ya Vinicius Jr.
Dakika ya 58, Valverde aliongeza bao la nne kwa Madrid ambalo ni la pili kwake katika mechi hiyo baada ya kuunganishiwa pasi na Carvajal lakini Hilal wakafufua matumaini kwa kuandika bao la pili lililofungwa na Vietto kwa pasi ya Abdulhamid.
Vinicius Jr kwa mara nyingine alifunga bao la pili katika mechi hiyo na la tano kwa timu yake katika dakika ya 69, bao lililotokana na pasi ya Ceballos.
Hilal pamoja na kuwa nyuma kwa mabao matatu lakini waliendelea kupambana na juhudi zao zilizaa matunda dakika ya 79 baada ya Vietto tena kuipatia timu yake bao la tatu ambalo ni la pili kwake katika mechi hiyo akiitumia vizuri pasi ya Delgado de Oliveira.
Hadi kufikia hatua hiyo, Madrid iliitoa Al Ahly ya Misri kwa mabao 4-1 katika nusu fainali wakati Hilal wao waliibwaga Flamengo ya Brazil na hivyo kuwa timu ya kwanza ya Saudi Arabia kucheza mechi ya fainali ya Kombe la Klabu la Dunia.
Kimataifa Real Madrid mabingwa wa dunia
Real Madrid mabingwa wa dunia
Read also