Na mwandishi wetu
Timu ya Yanga imerejea leo mazoezini kujiandaa na mchezo wa hatua ya 32 bora ya Kombe la FA dhidi ya Rhino Rangers ya Tabora utakaopigwa Jumapili hii kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Nasreddine Nabi amesema wamerejea mapema kujipanga kwani wanatakiwa kufanya kazi ya ziada kutetea taji hilo ukizingatia pia wana ratiba ngumu kwenye michuano ya Ligi Kuu NBC licha ya kuwa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.
Yanga inayoongoza ligi kwa pointi 56 dhidi ya mahasimu wao, Simba wanaoshika nafasi ya pili kwa pointi 50, imerejea kwenye maandalizi hayo ikiwa ni siku moja imepita tangu waibuke na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa.
Kocha huyo alieleza miongoni mwa mambo wanayoyaangalia na kuyafanyia kazi kwa sasa ni muunganiko wa wachezaji wapya waliotua hivi karibuni kwenye usajili wa dirisha dogo pamoja na wale waliokuwepo tangu awali ili kuendeleza ufanisi mkubwa ndani ya kikosi hicho.
“Ni wiki ya maandalizi makubwa kwa sababu ya ratiba iliyopo mbele yetu, kila mmoja ndani ya timu kuwa makini kutopoteza mechi hasa tukiwa tunapambana kutetea mataji ya ligi na FA, kufikia hayo lazima tuwe makini kwa benchi la ufundi kuandaa mfumo na muunganiko mzuri wa wachezaji wapya na waliokuwepo tangu mwanzo wa msimu,” alisema Nabi.
Alisema hali ya wachezaji wake iko vizuri akiwemo Kennedy Musonda ambaye alipata shida katika mechi iliyopita ya ligi lakini pia Khalid Aucho ambaye ameripotiwa kuanza mazoezi mepesi naye yuko katika mipango ya mchezo ujao dhidi ya Rhino inayotoka mkoani Tabora.