Na mwandishi wetu
Yanga imewatuliza mashabiki wake kwa kuichapa Ihefu bao 1-0 huku Azam ikiipa Tanzania Prisons kipigo cha nguvu kwa kuichapa mabao 3-0. Mechi zote hizo za Ligi Kuu NBC zimechezwa Jumatatu hii.
Itakumbukwa Novemba 29 mwaka jana Ihefu iliichapa Yanga mabao 2-1 na hivyo kuitibua dhamira ya timu hiyo iliyokuwa ikielekea kuweka rekodi ya kutopoteza mechi 50 mfululizo (unbeaten 50).
Baada ya kulala mbele ya Ihefu Yanga ikajikuta ikiishia na rekodi ya kutopoteza mechi 49 (unbeaten 49) chanzo ikiwa ni timu hiyo kutoka Mbarali.
Bao pekee la Yanga katika mechi yake na Ihefu iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam lilipatikana katika dakika ya 66 mfungaji akiwa mshambuliaji wake Fiston Mayele ambaye sasa anakuwa amefikisha mabao 15 akimuacha kwa mbali Moses Phiri wa Simba mwenye mabao 10.
Ushindi huo pia unaifanya Yanga kuendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ikiwa imefikisha pointi 53 ikiwaacha mahasimu wao Simba katika nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi tisa.
Yanga ambayo pia iliitumia mechi hiyo kumuonjesha kwa mara ya kwanza ladha ya Ligi Kuu NBC msimu wa 2022-23, mshambuliaji wake mpya, Kennedy Musonda, hadi sasa imecheza mechi 20, Simba imecheza mechi 19 na Jumatano itajitupa uwanjani kukabiliana na Mbeya City.
Azam nayo kwa ushindi huo uliopatikana nyumbani Chamazi Complex kwa mabao ya Yona Amos dakika ya tano, Abdul Sopu dakika ya 48 na Kipre Junior dakika ya 67 unaifanya timu hiyo kuendelea kujiimarisha katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 43 katika mechi 20 ikizidi kuisogelea Simba inayoshika nafasi ya pili.
Soka Mayele ailiza Ihefu, Azam yatoa kipigo
Mayele ailiza Ihefu, Azam yatoa kipigo
Related posts
Read also