Sao Paolo, Brazil
Mfalme wa soka na mwanasoka bora wa karne, Pele ambaye pia anatajwa kuwa ndiye mwanasoka bora wa wakati wote duniani, amefariki dunia kwa maradhi ya saratani.
Pele anatajwa kuwa na rekodi ya kufunga mabao 1,281 katika mechi 1,363 katika miaka yake 21 ya soka la ushindani akiwa pia na rekodi ya kuichezea timu ya Taifa ya Brazil mechi 77 na kuifungia mabao 92 na kuisaidia kubeba Kombe la Dunia mara tatu kuanzia mwaka 1958, 1962 na 1970 akiwa mchezaji pekee duniani aliyebeba taji hilo mara tatu.
Mwaka 2000 Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa ) lilimtangaza Pele kuwa mwanasoka bora wa karne na wakati maandalizi ya mazishi yake yakiendelea, Rais wa Brazil, Jair Bolsonaro ametangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa.
Katika miaka ya karibuni, Pele amekuwa akisumbuliwa na maradhi ya saratani na Septemba mwaka jana alifanyiwa upasuaji ili kuondoa uvimbe utomboni, upasuaji uliofanyika katika Hospitali ya Albert Einstein mjini Sao Paulo na kuendelea na matibabu ya kawaida ya kila mwezi lakini Novemba mwaka huu alirudishwa hospitali baada ya hali kuwa mbaya.
Mtoto wa Pele, Kely mara kadhaa amekuwa akitoa taarifa za kuugua kwa baba yake na kuonyesha matumaini lakini siku chache kabla ya sherehe za Krismasi alikiri kwamba mwanasoka huyo wa zamani alihitaji uangalizi wa karibu na hivyo familia ilikuwa naye pamoja wakati wa Krismasi kabla ya kufariki dunia usiku wa kuamkia leo Ijumaa akiwa na miaka 82.
Taarifa ya Kely aliyoitoa jana Alhamisi ilikuwa ya majonzi baada ya kutangaza kufariki kwa gwiji huyo wa soka pale aliposema, “kwa yote tunakushukuru wewe, tutakupenda bila ukomo, Pumzika kwa Amani.”
Shirikisho la Soka Brazil katika taarifa yake lilimtaja Pele kuwa ni mtu ambaye alikuwa zaidi ya mwanamichezo mkubwa wa wakati wote.
“Mfalme wetu wa soka alikuwa bingwa wa mafanikio ya Brazil, hakuwahi kuogopa kukabiliana na ugumu, alimuahidi baba yake Kombe la Dunia na akatupa sisi kombe hilo mara tatu, ahsante Pele.” ilieleza taarifa ya Shirikisho la Soka Brazil.
“Mfalme alitupa Brazil mpya na tunamshukuru mno kwa urithi huo, ahsante Pele,” ilifafanua sehemu ya taarifa ya shirikisho hilo.
Klabu ya zamani wa Pele ya Santos ilitoa taarifa za mazishi ikieleza kwamba Jumatatu mwili wa gwiji huyo utatolewa hospitali na kupelekwa kwenye Uwanja wa Urbano Caldera na kuwekwa katikati kwa ajili ya mashabiki kutoa salamu zao za mwisho.
Siku inayofuata Jumanne jeneza lenye mwili wa mchezaji huyo litapitishwa katika mitaa ya Santos mjini Sao Paulo kuelekea kwenye shughuli za mazishi zitakazoongozwa na wanafamilia.
Pele ambaye jina lake halisi ni Edson Arantes do Nascimento alianza kung’ara kwenye soka akiwa na miaka 17 akiisaidia Brazil kubeba taji la Dunia mwaka 1958, akikumbukwa zaidi kwa kupiga hat trick katika mechi ya nusu fainali dhidi ya Ufaransa na kuipeleka timu hiyo kwenye hatua ya fainali kabla ya kubeba taji likiwa ni taji lake la kwanza la dunia.