Doha, Qatar
Mshambuliaji wa England, Harry Kane anaandamwa na ukame wa mabao kwenye fainali za Kombe la Dunia wakati leo Jumapili timu yake inaumana na Senegal katika mechi ya hatua ya mtoano.
Kane ambaye pia ndiye nahodha wa England, mbali na kuandamwa na ukame wa mabao lakini pia ameandamwa na balaa la majeruhi ingawa leo anatarajia kuwa fiti kukabilina na wawakilishi hao wa Afrika katika mechi itakayoamua timu ya kufuzu robo fainali.
Baada ya kuandamwa na janga la kuwa majeruhi, Kane ameonyesha dalili zote za kuwa fiti kwa ajili ya mechi ya leo na ingawa hana bao hata moja lakini anajivuna kuwa na asisti tatu zilizochangia kuifanya timu hiyo imalize Kundi B ikiwa kinara.
Ukame wa mabao kwa Kane ni jambo gumu kwa mashabiki wa England kuamini kutokana na matumaini waliyokuwa nayo kwa mshambuliaji huyo ambaye kwenye fainali za Kombe la Dunia 2018 nchini Urusi alikuwa kinara wa mabao kwa kutupia kambani mara sita kabla ya England kutolewa na Croatia katika hatua ya nusu fainali.
Katika fainali za Euro 2020, Kane alifunga katika kila hatua ya mtoano ya michuano hiyo hadi England ikafikia hatua ya fainali na kushindwa kufurukuta mbele ya Italia ambao waliibuka vinara kwa mikwaju ya penalti.
Akiizungumzia mechi yao na Senegal Kane alisema, “muda utasema kila kitu, natumaini naweza kufanya vizuri kesho (leo) na kuwa katika kiwango bora kwa mechi za mtoano. Kuhusu kiwango najiona nacheza vizuri, mabao ndio kitu ninachofanyiwa tathmini na wengi lakini kama kawaida yangu, mimi ni mtulivu na wakati wote naingalia timu na kufanya kila kilicho bora kwa ajili ya timu.
Kwa upande wa Senegal habari za jana hazikuwa nzuri baada ya kuelezwa kuwa kocha wa timu hiyo, Aliou Cisse hakuweza kujumuika kwenye mazoezi na timu yake kwa siku mbili na hakushiriki katika mkutano na waandishi wa habari jana Jumamosi.
Msaidizi wake, Regis Bogaert, alipoulizwa alisema, “Joto limeongezeka mwilini kwa hiyo tulilazimika kuwa makini naye, tunatarajia kesho (leo) ataweza kuja na kuwa kwenye benchi na wachezaji, tuna hakika na hilo, atakuwa na timu.”
Nje ya hilo, Senegal licha ya kumkosa mshambuliaji wake nyota Sadio Mane ambaye ni majeruhi pamoja na kiungo wa Everton, Idrissa Guaye ambaye anatumikia adhabu, timu hiyo ina mastaa wengine nyote tegemeo kuanzia golini wana kipa tegemeo, Eduoard Mendy, kipa ambaye umahiri wake ameudhihirisha katika klabu ya Chelsea.
Katika safu ya ulinzi pia nyota mwingine wa Chelsea, Kalidou Koulibaly naye ni mchezaji mwenye uwezo na anayeongeza uzoefu utakaowapa tabu England katika mechi ya leo.
Kiujumla Senegal inatarajia kuwa timu tishio na mpinzani mkali wa kwanza wa England ikiwa ni timu yenye kujiamini ikiwa tayari imetoka kudhihirisha uwezo wake kwa kulitwaa taji la Mataifa ya Afrika na kufuzu kwa kishindo fainali za Kombe la Dunia ikiibwaga Misri.
Ukiiangalia England na matarajio makubwa yaliyo mgongoni mwake picha inayokuja ni kwamba timu hiyo ina kazi ngumu mbele ya Senegal itakayoingia uwanjani ikiwa na silaha moja kubwa ya kujiamini dhidi ya timu ambayo huenda ikajikuta ikicheza kwa presha.
Mechi za leo Jumapili hatua ya mtoano…
Ufaransa v Poland
England v Senegal
Kimataifa Kane kufuta ukame wa mabao?
Kane kufuta ukame wa mabao?
Related posts
Read also