Na mwandishi wetu
Simba leo Jumapili imeibuka kidedea kwenye Uwanja wa Ushirika mjini Moshi baada ya kuichapa Polisi Tanzania mabao 3-1 wakati Azam ikiwa Chamazi imetoka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Coastal Union katika mechi za Ligi Kuu NBC.
Nahodha John Bocco ambaye kwa sasa yuko kwenye kiwango bora, ndiye aliyefungua ukurasa wa mabao ya Simba katika dakika ya 33 kabla ya Moses Phiri kuandika bao la pili dakika moja kabla ya timu hizo kwenda mapumziko na kuifanya Simba ikamilishe dakika 45 ikiwa mbele.
Dakika tisa baada ya kuanza kipindi cha pili, Simba iliandika bao la tatu, mfungaji akiwa ni Phiri tena ambaye sasa anakuwa amekoleza vita ya kuwania tuzo ya mfungaji bora wa ligi hiyo na mabao yake manane akiwa ametanguliwa na Fiston Mayele wa Yanga mwenye mabao 10.
Hamisi Zuberi alifanikiwa kuipunguzia Polisi aibu baada ya kuifungia bao lao pekee lililopatikana katika dakika ya 90 ya mchezo huo.
Nao Azam wakiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam waliweza kuutumia vyema uwanja huo kwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Coastal Union.
Mabao ya washindi Azam yalifungwa na James Akaminko, Yahya Zayid na Iddi Nado wakati mabao ya Coastal yalifungwa na Maabad Maulid na Hamad Majimengi.
Matokeo ya leo yanaifanya Simba kufikisha pointi 31 katika michezo 14 ikiwa imetanguliwa na Azam yenye pointi 32 ambayo inashika nafasi ya pili nayo ikiwa imecheza michezo 14 kama Simba wakati Yanga ambayo pia ina pointi 32 ndiyo kinara wa ligi hiyo ikineemeka na wastani mzuri wa mabao ya kufunga lakini imecheza michezo 12.
Soka Simba, Azam zatamba
Simba, Azam zatamba
Related posts
Read also