Doha, Qatar
Cristiano Ronaldo leo Alhamisi ameweka rekodi mpya katika historia ya fainali za Kombe la Dunia kwa kuwa mchezaji wa kwanza kufunga kwenye fainali tano za michuano hiyo, katika mechi ambayo wawakilishi wa Afrika, Ghana wamejikuta wakifa kiume kwa kuchapwa mabao 3-2 na Ureno.
Ronaldo mwenye umri wa miaka 37 akiwa ndiye nahodha wa Ureno, alifunga bao lake katika dakika ya 65 kwa mkwaju wa penalti na hilo kuwa bao lake la 118 na timu ya Ureno, timu ambayo ameichezea mara 18 katika mechi za fainali za Kombe la Dunia.
Ghana walipambana na kusawazisha bao hilo dakika nane baadaye mfungaji akiwa Andrew Ayew, bao ambalo lilidumu kwa dakika tano baada ya Ureno kuongeza bao la pili mfungaji akiwa ni Joao Felix kabla ya Rafael Leao kuongeza bao la tatu kwa Ureno.
Ghana hata hivyo hawakukata tamaa na juhudi zao zilizaa matunda katika dakika tisa za nyongeza baada ya Osman Bukhari kuujaza mpira wavuni kwa kichwa na kuipatia timu hiyo bao la pili.
Baada ya bao hilo, kipa wa Ureno, Diogo Costa nusura aizawadie Ghana bao alipouweka mpira chini bila kujua kwamba mshambuliaji wa Ghana, Inaki Williams alikuwa nyuma yake lakini wakati akiuwahi mpira huo, Williams aliteleza na mpira alioupiga ulikuwa dhaifu na kuokolewa.
Akizungumzia bao lake la kwenye fainali za tano za Kombe la Dunia, Ronaldo alisema, “Ni tukio zuri katika fainali zangu za tano za Kombe la Dunia, nina furaha na hii timu kwa namna ilivyocheza vizuri, tumeshinda, tulianza vizuri, ni ushindi muhimu, tunajua kwamba katika mashindano haya kushinda mechi ya kwenye ni kitu muhimu.”
Kwa ushindi huo, Ureno sasa ndiyo inayoongoza Kundi H baada ya Uruguay na Korea Kusini, timu nyingine za kundi hilo kutoka sare ya bila kufungana.
Wawakilishi wengine wa Afrika, Cameroon nao walishindwa kutamba mbele ya Switzerland baada ya kuchapwa bao 1-0.
Kimataifa Ghana yafa kiume, Ronaldo aweka rekodi
Ghana yafa kiume, Ronaldo aweka rekodi
Related posts
Read also