Na mwandishi wetu
Mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele ameshukuru kufunga mabao matatu (hat-trick) ya kwanza tangu atue kwenye Ligi Kuu Bara, akifafanua pia jinsi gani alivyokuwa hajiskii vizuri kwa kukaa zaidi ya mechi tano bila kufunga.
Mayele alifunga mabao matatu jana katika ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Singida Big Stars ikiwa zimepita mechi tano za ligi bila kufunga huku zikiwa mechi saba za michuano yote.
Mchezaji huyo alisema kabla ya kufunga jana, alikuwa akipitia kipindi kigumu kwa kuwa hatimizi jukumu lake kama mshambuliaji ingawa anashukuru wachezaji wenzake walikuwa wakimpa moyo kwamba asijali ipo siku atafunga tena na kweli amefanya hivyo.
“Ni changamoto kwa sababu mimi kama mshambuliaji najitahidi lazima kila mechi nifunge, sasa mechi tano sijafunga sikuwa na furaha kabisa lakini timu nzima wakawa wananieleza kwamba nitafunga tu na hilo litakuja lenyewe kwa sababu wamezoea kuniona nafanya hivyo.
“Hata hii mechi ilikuwa ngumu lakini wachezaji tulijituma na nashukuru kwa matokeo hayo tukarudi kileleni na mimi pia nikarejea kileleni, wapo waliosema mwezi mzima sijatetema sasa, lakini nashukuru baada ya hapo nimefunga hat-trick yangu ya kwanza katika ligi Tanzania,” alisema Mayele.
Mayele raia wa Jamhuri ya Demokrasi ya Congo aliyetua Yanga msimu uliopita akitokea AS Vita, sasa amefikisha mabao sita sawa na Moses Phiri wa Simba, Idris Mbombo (Azam) na Reliants Lusajo (Namungo) ambao wako nyuma ya Sixtus Sabilo wa Mbeya City mwenye mabao saba.
Soka Hat-trick yamtuliza Mayele
Hat-trick yamtuliza Mayele
Related posts
Read also