Na Jonathan Haule,
Katika Filamu ya Huba juma hili tumeona jinsi mtego wa Tesa ulivyofanikiwa, hatimaye Chidi anakutana na mkewe Happy ana kwa ana nyumbani kwa JB.
Chidi anaonyeha hali ya kuchanganyikiwa baada ya kumuona Happy na kujaribu kuwa mkali akisaidiwa na Carlos katika kuwatisha Happy na JB lakini muda mfupi baadaye Chidi ananywea na kuwa mnyonge, anaanza kumbembeleza Happy ili aachane na JB.
Wakati yote hayo yakiendelea, Tesa anaonyesha furaha yake na kuanza kumsakama JB kwa maneno ya dhihaka akimshangaa mtu mzima kuingilia ndoa za watoto wadogo.
Cheko la Tesa linamuibua Nelly, binti wa pekee wa tajiri JB, Nelly anamshangaa Tesa kwa kicheko cha dharau na kuhoji nini hasa kilichomfanya acheke namna hiyo, kauli ya Nelly inamuibua Nicole ambaye anamtetea Tesa kwa namna alivyocheka na kumtaka Nelly anyamaze kama haoni cha kucheka.
Wakati yote hayo yakiendelea JB anaonekana kuwa kimya wakati Happy akijisogeza mithili ya mtoto wa swala mwenye hofu ya kuvamiwa na fisi, anajiweka karibu zaidi na JB ambaye wakati yote hayo yakiendelea amekuwa kimya.
Kimya cha JB kinaacha maswali, ni kama vile yupo mtegoni, anasoma mazingira kabla ya kuchukua maamuzi. Je nini atakifanya kwa Happy, na nini atakifanya kwa Chidi na Carlos, na nini atakifanya kwa Nicole na Tesa ambao wote ni kama wavamizi waliovamia nyumbani kwake?
Sehemu ya utamu wa Filamu ya Huba itaanzia hapo, maswal yote hayo au baadhi yake hapana shaka majibu yake yatapatikana Jumatatu hii usiku.
Hapo hapo bado kuna swali kuhusu Nicole na Tesa, wote wanajua raha ya kuwa na JB, mpenzi tajiri, tena tajiri anayejua kudhihirisha jeuri ya fedha zake pale anapopenda, hakuna kati yao anayefurahia kulikosa penzi la aina hiyo ambalo Happy mtu wanayemuona hana hadhi hiyo ndiye aliyechaguliwa na JB kulifurahia penzi la aina hiyo.
Katika mazingira yote hayo swali ambalo halijapata jibu juma lililopita linaendelea kubaki vile vile, swali hilo ni je urafiki wa Tesa na Nicole ambao kimsingi unaweza kusema ni urafiki wa dharura, utadumu iwapo JB ataamua kuachana na Happy? Au wataingia katika vita mpya ya kumtaka JB?
Dave naye bado yuko njia panda kama ndugu yake Roy, uamuzi wake wa kwenda kujituliza kwa Kibibi umekuwa mgumu, Kibibi anamapenzi yasiyoeleweka lakini kubwa ni ukali na ukatili ambao amekuwa akiudhihirisha kwa Dave, licha ya kulala chumba kimoja na kuonekana akiji-baby-isha kwa Dave lakini hakuchelewa kumgeuka na kumdhihirishia alivyo mwanamke mbabe asiyechezewa.
Mazingira hayo yanamfanya Dave azidi kuchanganyikiwa na hatimaye anaamua kumrudia Tima lakini hapo hapo anakutana na mtihani mwingine, Nelly hatimaye anaamua kutumia ushirikina pengine kwa lengo la kumtoa Dave kwa Tima, anachinja kuku wa kienyeji mwenye madoadoa na kumuweka kwenye geti la kuingia nyumbani kwa Tima, pengine ni kwa maelekezo ya mganga wa kienyeji.
Katika hali ambayo haikutarajiwa Dave anakutwa eneo hilo hilo akiwa amemshika kuku huyo katika hali ya mshangao, ghafla Tima naye anafungua geti lake na kumkuta Dave akiwa amemshika kuku huyo na moja kwa moja anaamini Dave ndiye aliyemuweka kuku eneo hilo.
Dave anafukuzwa kama mwizi nyumbani kwa Tima, anaamua kuondoka akiwa katika hali ya unyonge na aliyevurugwa kwa kuhusishwa na ushirikina ambao hakuufanya.
Nini hatma ya Dave na Tima? Je Tima atamsamehe kwa sababu tusisahau ukweli kwamba anampenda, na je Dave atafanya nini baada ya Tima kumfukuza, ataendelea kujishikiza kwa Kibibi au ataamua aende kwa Nelly ambaye pia anampenda sana Dave na haoni wala hasikii.
Dave katika Filamu ya Huba amefanikiwa kufikisha ujumbe wa mwanaume aliyevurugwa na wapenzi na ambaye pia amekosa msimamo.
Kwa Doris na mama yake Bi Sikitu nako hali inazidi kuwa tete, Doris bado hana amani baada ya kusikia mke mwenzake Nandi ana mtoto, anatangaza azma yake ya kwenda Pemba jambo ambalo Bi Sikitu licha ya kubobea katika ushirikina lakini anamuonya kwamba Pemba si mchezo, anamtaka asijaribu kwenda kwa sababu waganga wa Pemba si mchezo.
Dorisi anaamua kumpuuza mama yake na kusisitiza kwamba lazima aende Pemba, mumewe Roy naye ni kama vile ameshindwa kumzuia mkewe asiende Pemba. Je nini kitatokea kuhusu mpango wa Doris, na je mumewe Roy atafanya nini? Ni majibu ambayo yataanza kupatikana kuanzia Jumatatu hii.