London, England
Timu 12 zimeshafuzu hatua ya mtoano Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) wakati hatma ya timu nne itajulikana katika mechi za leo Jumanne na kesho Jumatano ili kupata timu 16, kazi ngumu ipo Kundi D lenye timu za Tottenham, Sporting Lisbon, Eintracht Frankfurt na Marseille.
Tottenham licha ya kuongoza kundi hilo lakini kufuzu kwake bado kupo njia panda, leo itaumana na Marseille katika mechi ambayo ni lazima ishinde ili iongoze kundi na kufuzu moja kwa moja, tofauti na hivyo inaweza kuangukia Europa Ligi au kuaga moja kwa moja mashindano ya Ulaya msimu huu.
Kibaya zaidi ni kwamba katika mechi hiyo Tottenham itakuwa uwanjani bila ya kocha wake Antonio Conte ambaye anatumikia adhabu aliyopewa wiki iliyopita katika mechi dhidi ya Eintracht Frankfurt badala yake kazi yake itafanywa na msaidizi wake, Cristian Stellini.
Kiujumla hatma ya timu zote za kundi hili itajulikana baada ya mechi zao za leo za kufunga hesabu za kundi hilo na hivyo haitokuwa ajabu kwa Tottenham ama kuangukia Europa Ligi au kuaga moja kwa moja michuano ya Ulaya msimu huu.
Katika mechi za leo za Kundi D, Tottenham inayoongoza kundi hili ikiwa na pointi nane inaweza kupitwa na Marseille inayoshika mkia ikiwa na pointi sita wakati Sporting Lisbon inayoshika nafasi ya pili ina pointi saba na Eintracht Frankfurt inashika nafasi ya tatu nayo pia ikiwa na pointi saba.
Ili Tottenham ifuzu inahitaji sare katika mechi ya leo na Marseille ingawa ushindi utawafanya si tu wafuzu bali wafuzu wakiwa vinara wa kundi hili. Ni hivyo hivyo kwa Sporting Lisbon nayo ili ifuzu inahitaji sare katika mechi yake ya leo na Eintracht Frankfurt.
Kushindwa kwa timu mojawapo kati ya hizo kunaweza kuwatupa hadi nafasi ya tatu au ya nne kutegemea na matokeo mengine na kwa Tottenham pia ikitokea ikashindwa leo inaangukia nafasi ya tatu na kujikuta ikicheza Europa Ligi na kuziacha Sporting na mojawapo kati ya Eintracht Frankfurt na Marseille zikifuzu.
Kundi A
Katika Kundi A Napoli na Liverpool zimeshafuzu, Liverpool leo itaumana na Napoli wakati Benfica itacheza na Ajax, mechi ambayo Liverpool na Napoli zitakuwa zikipigania kushika usukani wa kundi hilo.
Napoli inaongoza kundi hilo ikiwa na pointi 15 wakati Liverpool ina pointi 12, mshindi katika mechi ya leo atakuwa na nafasi ya kuwa kinara wa kundi ingawa kwa Napoli matokeo yoyote ya sare yanatosha kuwafanya washike usukani wakati Liverpool itatakiwa kushinda kwa mabao manne au zaidi ili iweze kumaliza ikiwa kinara wa kundi hilo.
Kwa Rangers ili iangukie kwenye Europa Ligi nayo inahitaji kuifunga Ajax mabao matano au zaidi tofauti na hivyo timu hiyo nayo inaaga rasmi michuano ya Ulaya kwa msimu huu na kuiacha Ajax ikiangukia kwenye Europa Ligi.
Kundi B
FC Porto na Club Bruges zimeshafuzu Kundi B na zote leo zinacheza mechi zao za mwisho kupigania kushika usukani wa kundi hilo, Bruges wana pointi 10, Porto wana pointi tisa na leo Bruges wanacheza na Bayer Leverkusen wakati Porto wanacheza na Atletico Madrid kukamilisha mechi zao za makundi.
Mbio za kuangukia Europa katika kundi hili zipo wazi kwa Atletico Madrid yenye pointi tano na Bayer Leverkusen yenye pointi nne, timu zote hizo zinahitaji kushinda mechi ya leo ili kujiweka pazuri ingawa Atletico Madrid itakuwa imejiweka pazuri iwapo itapoteza kama Leverkusen nayo itapoteza kwani wanachoshindania ni wingi wa pointi.
Kundi C
Hili ni kundi ambalo limemaliza hesabu zake, Bayern Munich imeshafuzu ikiwa kinara wa kundi na pointi zake 15 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote wakati Inter Milan inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 10 ambazo haziwezi kufikiwa na Barcelona inayoshika nafasi ya tatu ikiwa na pointi nne na Viktoria Plzen pia inayoshika mkia ikiwa haina pointi hata moja.
Kwa hiyo Bayern na Inter zinasonga hatua ya mtoano wakati Barca imeangukia Europa Ligi na Viktoria imeaga rasmi michuano ya klabu barani Ulaya kwa msimu huu.
Kundi E
Kundi E nalo limekaa kimtego ingawa kwa Chelsea tayari imefuzu ikiwa na pointi 10 kazi ipo kwa AC Milan yenye pointi saba ambayo inahitaji sare ili iungane na Chelsea vinginevyo inaangukia nafasi ya tatu na kucheza Europa Ligi. Katika mechi za mwisho za kundi hili zitakazochezwa kesho, Milan itaivaa Salzburg wakati Chelsea itaumana na Dinamo Zagreb.
Salzburg ina pointi sita ikiifunga Milan itafikisha pointi tisa na kuiacha timu hiyo wakati Zagreb nayo ikiifunga Chelsea itafikisha pointi saba sawa na Milan. Zagreb yenye pointi nne nayo inaweza kuangukia kwenye Europa Ligi iwapo itaifunga Chelsea na kuombea Salzburg ifungwe na Milan.
Kundi F
Katika Kundi F, Real Madrid tayari imefuzu ikiwa na pointi 10 na kesho itaumana na Celtic kumalizia mechi yake ya hatua ya makundi ikisaka pointi za kuiwezesha kushika usukani wa kundi hilo, nafasi ambayo pia inaweza kushikwa na Leipzig yenye pointi tisa.
Wakati Celtic ikiwa tayari imeaga michuano ya Ulaya msimu huu na pointi zake mbili, Shakhtar Donetsk yenye pointi sita inaweza kushika nafasi ya pili iwapo itaifunga Leipzig na hivyo kufikisha pointi tisa sawa na Leipzig na moja ya timu hizo kuneemeka na mabao ya kufunga na kufungwa.
Kundi G
Hesabu za kundi hili zimekamilika na kesho zitaingia uwanjani kukamilisha ratiba, Man City inaongoza kundi hili ikiwa na pointi 11 ikifuatiwa na Borussia Dortmund yenye pointi nane, timu hizo zote zimefuzu wakati Sevilla ingaangukia kwenye Europa Ligi ikiwa na pointi zake tano na FC Copenhagen inaaga rasmi michuano ya Ulaya msimu huu ikiwa na pointi zake mbili.
Katika mechi zao za mwisho za makundi, Man City itaumana na Sevilla wakati FC Copenhagen itatoana jasho na Borussia Dortmund.
Kundi H
Vigogo wa Paris, klabu ya Paris Saint Germain au PSG tayari wamefuzu wakiwa vinara wa kundi hadi sasa na pointi zao 11 wakifuatiwa na Benfica ambayo pia ina pointi 11, pointi ambazo haziweza kufikiwa na Juventus na Macabi Haifa ambazo kila moja ina pointi tatu.
Katika mechi za mwisho za kundi hili hapo kesho, Benfica inaweza kushika usukani iwapo itaifunga Maccabi huku ikiombea PSG ipoteze mechi yake na Juventus lakini PSG nayo ikishinda itashika usukani, kila mmoja ataombea mwenzake apoteze.
Vita ipo kwenye Europa Ligi, Juventus na Maccabi, yeyote atakayeshinda atakuwa ameangukia katika ligi hiyo huku akiombea mwenzake apoteze na kama timu hizo zitafungana pointi tofauti ya mabao na mechi baina ya timu hizo itakuwa na maana kubwa kwa timu zote za kundi H.
Zilizofuzu mtoano UCL
Liverpool, Napoli, Club Bruges, FC Porto, Bayern Munich, Inter Milan, Chelsea, Real Madrid, Man City, Borussia Dortmund, PSG na Benfica.
Mechi za Ligi ya Mabingwa leo Jumanne…
Liverpool v Napoli
Rangers v Ajax
B.Leverkusen v Club Bruges
FC Porto v Atl Madrid
Bayern Munich v Inter Milan
Viktoria Plzen v Barcelona
Marseille v Tottenham
S. Lisbon v E. Frankfurt
Kesho Jumatano
Chelsea v Dinamo Zagreb
AC Milan v Red Bull Salzburg
Real Madrid v Celtic
Shakhtar Donetsk v RB Leipzig
FC Copenhagen v B.Dortmund
Man City v Sevilla
Juventus v PSG
Maccabi Haifa v Benfica