Na mwandishi wetu
Baada ya jana timu za Coastal Union na Geita Gold kutoka suluhu, makocha wa timu hizo wameonesha kuvutiwa na viwango vya wachezaji wao katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
Kocha wa Coastal, Yusuf Chipo alisema kwamba anasikitika wamepoteza pointi tatu muhimu lakini anashukuru hawakupoteza mchezo huo kwa vijana wake kuonesha soka safi lakini pia kwa kuwa wamemaliza bila kuwa na majeruhi.
“Tumepoteza pointi tatu lakini tumemaliza mchezo salama bila majeruhi, mchezo ulikua mgumu, tumepambana lakini kidogo hatukuwa vizuri kwenye kufunga kitu ambacho naamini tutakifanyia kazi, tutakaa sawa.
“Kiujumla nimeridhishwa na viwango vya wachezaji wangu lakini kama kocha huwezi kuridhika kupata sare nyumbani lakini naamini tungeweza kufanya bora zaidi ya hapo, tutazidi kukaa sawa,” alisema Chipo.
Naye Kocha wa Geita, Fred Felix Minziro aliwapongeza vijana wake hasa wa safu ya ulinzi ambayo haikuruhusu bao kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa ligi msimu huu.
“Nawapongeza vijana wangu, leo hii (jana) kwa mara ya kwanza ndani ya mechi sita wamecheza bila kuruhusu bao, naipongeza safu ya ulinzi na kule mbele pia kama tungejitahidi tungepata bao, nashukuru tumemaliza salama na tumeondoka na pointi moja tuliyokuja nayo,” alisema Minziro.
Hiyo ni mechi ya tatu mfululizo kwa Coastal inashindwa kutamba mbele ya Geita iliyopanda Ligi Kuu Bara msimu uliopita. Mechi ya kwanza Geita iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 kabla ya sare ya bao 1-1.
Soka Minziro, Chipo wazisifia Geita, Coastal
Minziro, Chipo wazisifia Geita, Coastal
Related posts
Read also