Na mwandishi wetu
Klabu ya Yanga sasa ipo huru kumtumia mshambuliaji wake, Twisila Kisinda baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitisha rasmi usajili wake baada ya awali kushindwa kuthibitisha usajili huo.
Taarifa iliyotolewa na TFF jioni hii kupitia kwa Kamati ya Hadhi na Wachezaji imeeleza kumruhusu mchezaji huyo baada ya klabu hiyo kumhamisha mchezaji wake wa kigeni, Lazarous Kambole raia wa Zambia waliyemsajili kutoka Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
Awali kuliibuka sintofahamu baada ya Yanga kumsajili Kisinda raia wa DR Congo ndani ya muda wa usajili lakini TFF ilizuia usajili huo ikieleza Yanga ilizidisha idadi ya wachezaji 12 wa kigeni iliokuwa nao.
Shirikisho hilo limefafanua kuwa baada ya Yanga kumhamisha Kambole aliyetimkia Wakiso Giants ya Uganda sasa imepata nafasi ya kumpitisha Kisinda na tayari Hati ya Uhamisho ya Kimataifa (ITC) ya mchezaji huyo aliyerejea Yanga kutoka RS Berkane ya Morocco imepashapatikana.
Kisinda aliwahi kuitumikia Yanga akitokea AS Vita ya Congo msimu wa 2020/21 na kuonyesha makali yaliyompeleka Berkane alikocheza kwa msimu mmoja chini ya Florent Ibenge na sasa timu hiyo ya Jangwani imemrejesha tena kuunganisha nguvu na kina Fiston Mayele, Stepahe Aziz Ki, Feisal Salum, Bernad Morrison na wengine kuhakikisha wanatetea ubingwa wa Ligi Kuu NBC msimu huu na kufanya vyema kwenye michuano ya Caf.
.