Na Jonathan Haule
Miaka saba imetimia tangu Banza Stone aage dunia, kuna mengi ya kumkumbuka, tukirudi miaka ya 1990 mwishoni, tuukumbuke usiku mmoja mwishoni mwa wiki, sauti yake nzito inasikika ikitamka kwa madaha, ‘Pepetaa Pepetaaa, Pepetaa Pepetaaa, piga bao, ukitwanga lazima upepete..’.
Unapomtaja Banza Stone kuanzia miaka ya 1990 hasa mwishoni katika muziki wa dansi utakumbuka mengi, kwanza ni namna alivyoonyesha kipaji cha hali ya juu na kuchangia mafanikio ya bendi ya Twanga Pepeta katika muziki wa dansi.
Wakati huo bendi ya Diamond Sound au Wana Dar es Salaam Ikibindankoi ilikuwa juu, Allan Mulumba na wenzake waliifanya bendi hiyo iwe kimbilio la wapenzi wa muziki hasa ule wenye mahadhi ya DR Congo, ni bendi ambayo ilipunguza ziara za wanamuziki wa DR Congo nchini, ilionekana kama vile hakukuwa na tofauti kubwa kati ya Diamond Sound na bendi hizo.
Hapo hapo kukawa na Beta la Musica na bendi nyinginezo ambazo zilishindana katika soko la muziki nchini huku miondoko na midundo ya DR Congo ikitawala katika ushindani huo.
Ni kipindi hicho hicho hasa mwaka 2000 mwanzoni ndipo Twanga Pepeta nao wakaibuka na kuleta mapinduzi mapya, wakijipima msuli na bendi zilizosheheni wasanii wa DR Congo na hatimaye baadhi ya bendi hizo zikaanza kujifia na kutoweka. Mfano wakati Twanga Pepeta ikipata umaarufu na umaarufu wa Diamond Sound ulianza kushuka taratibu na hatimaye bendi hiyo kujifia, ile rapu yake ya ‘kutesa kwa zamu’ ni kama vile iliakisi kupanda kwa Twanga Pepeta na anguko la bendi nyingine.
Wakati harakati za uchaguzi mkuu wa mwaka 2000 zikipamba moto, Banza alitambulishwa mbele ya waandishi wa habari na mkurugenzi wa TOT, Kapteni John Komba kwamba anajiunga na TOT kwa kuazimwa ili akashiriki kampeni za uchaguzi za CCM.
Kilichotokea ni kwamba baada ya uchaguzi mkuu, Banza hakurudi tena Twanga, akabaki kuwa msanii wa bendi ya muziki ya TOT ambao walikuwa wakihaha kuutangaza mtindo wao wa Achimenengule.
Akiwa TOT ikawa fursa yake ya kuibadili bendi hiyo, alianza kuubadili muziki, wakati huo ungemsikia Banza akighani, ‘Achimenengule kibambaa’, akawavuta baadhi ya wasanii waliotamba kwenye taarab na kuwapa nafasi kwenye muziki wa dansi, nafasi ambazo walizimudu vyema mfano ni Abdul Misambano na marehemu Leila ambao walitamba katika kibao cha ‘Mtaji wa Masikini’.
Banza kisha akaisuka upya na kuiongezea nguvu bendi ya TOT kwa kuingiza wasanii wapya akiwamo muimbaji Waziri Sonyo, mpiga drums Gabby Katanga na wengineo ambao kwa pamoja waliunda TOT iliyoonekana kukamilika kila idara na labda kibao cha ‘Masimango’ utunzi wa Waziri Sonyo kilidhihirisha uwezo wa Banza na wenzake ndani ya TOT ya wakati huo.
Katika kibao cha Masimango ukianzia kwenye uimbaji sauti za Misambano, Waziri Sonyo, Toto Tundu na Banza mwenyewe na sauti yake nzito, kwa uchache tu vyote hivyo vilikolezwa na drums zilizopigwa kwa ufasaha na Gabby Katanga pamoja na gita lililovurumishwa na Elly Chinyama na wenzake.
Kibao cha Angurumapo Simba kilichompa umaarufu Banza akiwa Twanga akakifanyia remix akaingiza mashairi ya ‘Ni mimi Simba wala si ujinga na tena wakati nawinda we cheza mbali makida, Banza mwana wa Sinza, Sinza kwa wajanja, Achimenenguleee, njoo tunengue, Achimenenguleee, si wewe wala yule, Simba ana unguruma nchini Tanzania.’
Hadi hapo TOT ikajiona imepiga hatua na kuingia katika ushindani wa maneno na Twanga na hatimaye mpambano wa bendi hizo mbili ukaandaliwa kwenye Ukumbi wa Vijana, Twanga wakatawala mpambano na ingawa baadaye TOT walijinasibu kwamba bendi yao ilipiga muziki mzuri lakini mvuto wa wapenzi wa muziki ulilalia upande wa Twanga.
Kwa TOT kuwa tayari kwa mpambano na Twanga ilikuwa ni hatua moja kubwa ya kuonyesha namna walivyojiamini, kujiamini kulikotokana na kazi kubwa iliyofanywa na Banza.
Baada ya hapo wasanii wote wa TOT walipelekwa masomoni Chuo cha Sanaa Bagamoyo, na baada ya kurudi Banza akaja na kibao cha ‘Elimu ya mjinga ni majungu’ ni kazi nyingine iliyoonyesha nguvu ya kipaji chake katika muziki wa dansi, kibao ambacho alikinogesha na rapu yake ya ‘kitimtim’
Hiyo ikawa kama kazi yake kubwa ya mwisho ndani ya TOT, mgogoro wa chinichini ukaanza kufukuta na mwishowe akaaga katika bendi hiyo jambo ambalo lilionekana kutomfurahisha Kapteni John Komba ambaye licha ya kukubali kuondoka kwa msanii huyo lakini alisema kwamba alijitahidi kuishi naye kama mtoto wake.
Banza akaondoka TOT na kuanzisha bendi aliyoipa jina la Bambino Sound, bendi ambayo inadaiwa kulikuwa na watu nyuma yake lakini haikudumu ikasambaratika mapema jambo ambalo lilitabiriwa na baadhi ya watu waliodai kwamba pamoja na kuwa na kipaji kikubwa cha muziki lakini kwenye masuala ya uongozi hasa wa bendi, Banza asingeweza.
Na ingawa baada ya hapo alionekana katika bendi za Tam Tam na Extra Bongo, hadithi kubwa ikawa Banza ataelekea wapi, kati ya Twanga na TOT kwani kote bado alikuwa akihitajika, hatimaye akarudi Twanga.
Akiwa Twanga mara ya pili akaonyesha tena nguvu ya kipaji chake jambo ambalo linadhihirika katika kibao cha Mtu Pesa ambacho amekitawala vyema huku rapu yake ya ‘Shoka moja mbuyu chini’ ikiongeza utamu, rapu ambayo haikuishia kuwa burudani kwenye majukwaa ya muziki tu bali ilikuwa gumzo hadi mitaani kama ilivyokuwa huko nyuma kwenye vionjo alivyovipenda vya ‘kutesa kwa zamu’.
Ni baada ya kufurahia mafanikio ya safari ya pili ndani ya Twanga ndipo afya ya Banza ilipoanza kutetereka, habari za Banza anaumwa nini zikatawala vyombo vya habari, kwa kumuona tu ilitosha kutoa dalili kwamba msanii huyo alihitaji tiba ya tatizo lililokuwa likimkabili.
Jambo baya hata hivyo ni kwamba kila mtu alikuwa daktari akawa na ugonjwa wake pamoja na tiba huku wengine wakionekana kama kumsakama, Banza akahusishwa na magonjwa mengi kuanzia kifua kikuu na mengineyo huku wengine wakidai si mgonjwa bali aliponzwa na aina ya ulevi waliodai anautumia na ndio sababu hasa iliyomfanya adhoofike.
Ni dhahiri alikerwa na alichokuwa akisemwa au aliamua bora ajitabirie kifo, Banza akadhihirisha uwezo wake kwenye muziki kupitia kibao cha ‘Hujafa hujasifiwa’, ni kibao kinachotia huzuni, ni kama wimbo unaoimbwa na mtu aliyekata tamaa ya kuishi au kuchoshwa na tabia za wanadamu kumsimanga na kumzushia kifo, Banza katika wimbo huo anaizungumzia siku yake ya kifo itakavyokuwa nini watu watasema kama ambavyo sehemu ya mashairi ya wimbo huo yanavyojielezea…
‘Basi Namuomba Mungu anifanyie kama Yesu Masiha, alivyokufa baada ya siku tatu akafufuka, lakini kwangu Banza Stone mimi nasema haiwezekani, basi namuomba Mungu japo kwa sekundu moja ayafungue macho yangu na masikio yangu ili nipate kusikia watu wanasema nini hapa duniani, eeeh. Wengine utawasikia Banza anaimba sana, utawasikia Banza ni mzuri sana, utawasikia Banza ana sauti nzuri, utawasikia Banza anatunga sana na wambea watachonga teja hiloo linavuta ngoma…
Na ndicho kilichotokea, Julai 17, 2015, Ramadhan Ali Masanja tuliyemjua zaidi kwa majina ya Banza Stone, Mwalimu wa walimu au Jenerali akaaga dunia na huenda baada ya kifo chake wakati akilazwa kwenye Makaburi ya Sinza mengi yalizungumzwa yakiwamo mazuri na mabaya ya wambeya kama alivyosema katika kibao cha Hujafa hujasifiwa. Apumzike kwa amani.