Paris, Ufaransa
Aliyekuwa mchezaji na baadaye kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane amezungumzia mambo yake ya baadaye katika kazi ya ukocha. Sambamba na hilo amesema hajivunii kumpiga kichwa beki Mtaliano Marco Materazzi.
Zizou akiwa mchezaji tegemeo wa timu ya Taifa ya Ufaransa mwaka 2006 kwenye mechi ya fainali ya Kombe la Dunia nchini Ujerumani, anakumbukwa kumpiga kichwa Materazzi na kupewa kadi nyekundu na hatimaye Italia kushinda kwa mikwaju ya penalti na kutangazwa mabingwa wapya wa dunia.
Katika mechi hiyo, Zizou aliifungia Ufaransa bao kwa mkwaju wa penalti aliyoipiga kwa staili maarufu ya panenka lakini Materazzi alisawazisha na baadaye timu zikaenda kwenye mikwaju ya penalti ndipo, Italia walipoibuka vinara.
Mara baada ya kumpiga kichwa Materazzi na habari kuwa gumzo duniani kote, Zizou aliwahi kusema kwamba anasikitika watoto wadogo nao wameona akifanya jambo hilo.
“Sijivunii,” alisema katika mazungumzo yake na Telefoot kuhusu tukio hilo ambalo liliwahi kuwa mjadala mkubwa kuhusu sababu hasa ya Zizou kufanya alichofanya huku ikidaiwa kwamba Materazzi alimtolea lugha ya kumkashifu Zizou ambaye hiyo ilikuwa mechi yake ya mwisho kwani kabla ya hapo alitangaza angestaafu soka.
Kuhusu kazi ya ukocha, Zizou ambaye baada ya kuondoka Real Madrid kwa mara ya pili takriban mwaka mmoja uliopita, amekuwa hana klabu anayoinoa ingawa amekuwa akihusishwa na mipango ya kuinoa PSG ili kuziba nafasi ya Mauricio Pochettino.
Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron aliwahi kuzungumzia nia yake ya kumshawishi kiungo huyo wa zamani wa timu ya Taifa ya Ufaransa kuwa kocha katika moja ya klabu ya Ligi 1 nchini Ufaransa huku ikiaminika kuwa klabu hiyo ingekuwa PSG lakini Zizou mwenyewe alikanusha habari hizo na inadaiwa hajawa tayari kuinoa PSG.
Zizou ambaye akiwa kocha Real Madrid ameipa mataji matatu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, inadhaniwa kwamba anasubiria kibarua cha kuinoa timu ya Taifa ya Ufaransa kutokana na habari kwamba kocha wa sasa wa timu hiyo, Didier Deschamps anatarajia kuachana na timu hiyo mara baada ya fainali za Kombe la Dunia baadaye mwaka huu huko Qatar.
Akizungumzia hilo Zizou alisema, “Je bado nina uwezo wa kuchangia kitu nikiwa kocha, ndio, ninaweza kuchangia mengi au machache, nataka kuendelea na kazi ya ukocha kwa sababu shauku hiyo bado ipo, ni jambo ninalovutiwa nalo na tayari nina miaka 50 sasa, jambo moja la muhimu ni kwamba nina furaha.”
Kimataifa Zizou: Sijivunii kumpiga kichwa Materazzi
Zizou: Sijivunii kumpiga kichwa Materazzi
Related posts
Read also