Madrid, Hispania
Real Madrid ni kama wanaumia kwa kumkosa Kylian Mbappe, awali walidai kuna matumizi mabaya ya fedha na kuahidi kuishitaki PSG kwenye mamlaka za soka Ulaya, sasa wanadai shinikizo limetumika kumfanya mchezaji huyo abadili ndoto zake za kuichezea klabu hiyo.
Rais wa Real Madrid, Florentino Perez amenukuliwa akisema kwamba anaamini Mbappe ‘kalazimishwa’ kubadili ndoto yake ya kuichezea klabu hiyo ya Hispania.
Katika kipindi ambacho uvumi kuhusu usajili wa mchezaji huyo ukiwa juu huku ikiaminika angeachana na PSG na kujiunga na Real Madrid, ghafla aliamua kubaki PSG kwa mkataba unaotajwa kuwa mnono wa miaka mitatu..
“Ndoto yake ilikuwa ni kuichezea Real Madrid,” alinukuliwa Perez akisema kumzungumzia Mbappe, mshambuliaji mwenye umri wa miaka 23 ambaye ametokea kuwa tegemeo kwa PSG pamoja na timu ya Taifa ya Ufaransa.
“Tulitaka kumsajili Agosti mwaka jana lakini hawakumruhusu, alikuwa akisema mara kwa mara kwamba anataka kuchezea Madrid, siku 15 kabla kila kitu kikabadilika,” alisema Perez huku kukiwa na habari kwamba mchezaji huyo alikubaliana kila kitu na Real Madrid ikiwamo maslahi yake lakini ghafla akabadili msimamo akidai anataka kubaki PSG.
Akifafanua namna ambavyo Mbappe alibadilika, Perez alisema, “Huyu si yule Mbappe niliyetaka kumsajili, ni mwingine ambaye amebadili ndoto yake, amebadilika, ameahidiwa mambo mengine, ametiwa presha na tayari amekuwa mwanasoka mwingine tofauti. Mbappe aliyekuwa aje hapa si huyu, kama ni huyu napenda abaki huko PSG namtaka Mbappe mwenye ndoto ya kucheza Real Madrid.”
Kwa upande wake Mbappe bado hajafuta mpango wa kujiunga na Real Madrid kwa siku zijazo pale aliposema kwamba mpango huo upo na si kwamba umefikia mwisho.
Habari nyingine zinadai kuwa Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron naye alihusika katika kumshawishi mchezaji huyo abaki PSG kama ambavyo anadaiwa kumshawishi Zinedine Zidane ‘Zizou’ kuinoa PSG.
Kimataifa Madrid: Mbappe kashinikizwa abaki PSG
Madrid: Mbappe kashinikizwa abaki PSG
Related posts
Read also