Ni Real Madrid Ulaya
Real Madrid wameiteka dunia, ndivyo unavyoweza kusema kuhusu ushindi wa Jumamosi usiku wa bao 1-0 ambao timu hiyo iliupata dhidi ya Liverpool katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Usiku huo mashabiki wa soka duniani kote akili zao zilikuwa katika jiji la Paris ambapo mechi hiyo ilichezwa ili kumpata bingwa wa klabu barani Ulaya na hatimaye wababe wa michuano hiyo, Real Madrid wakafanikiwa kuibwaga Liverpool.
Lilikuwa ni bao la dakika ya 59 mfungaji akiwa ni Vinicius Junior ambaye aliitumia vizuri pasi ya Fede Valverde na kuvuruga ndoto za Liverpool kutwaa taji la saba la michuano hiyo na hivyo kuwa sawa na AC Milan ambayo inashika nafasi ya pili kwa kutwaa taji hilo mara nyingi.
Liverpool tangu mwanzo wa mchezo walionekana kuwa na ari ya kulibeba taji hilo walilolikosa mwaka 2018 katika fainali dhidi ya Real Madrid baada ya kuchapwa mabao 3-1 na safari hii walijipa matumaini kwamba huu ni wakati wao lakini bao la Vinivicius liliharibu kila kitu.
Katika mbio hizo, Real Madrid ina kila sababu ya kumshukuru kipa wao, Thibaut Courtois kwa kuokoa hatari nyingi zilizoelekezwa na wachezaji wa Liverpool ambao katika safu yao ya ushambuliaji walikuwa na vinara wao, Mane na Mohamed Salah.
Kabla ya mechi hiyo, Courtois alinukuliwa akisema kwamba Real Madrid inapofikia fainali inaibuka mshindi na hicho ndicho kilichotokea licha ya kujikuta akipingwa vikali kwenye mitandao ya kijamii kwa kauli hiyo.
Kwa Real Madrid hilo linakuwa taji lao la 14 wakiwa ndio wanaoongoza kwa kulibeba mara nyingi lakini linakuwa taji la nne kwa kocha wao Carlo Ancelotti ambaye huko nyuma aliwahi kulibeba mara mbili akiwa na AC Milan na sasa ameweka rekodi nyingine ya kulibeba mara mbili akiwa Real Madrid.
Kabla ya mechi hiyo kuliibuka utata kuhusu hali ya usalama na kusababisha Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa) kuchelewa kuanza mechi hiyo kwa dakika 36 huku polisi wakitumia mabomu ya machozi kuwadhibiti mashabiki wengi wao wakiwa wa Liverpool waliokuwa wakitaka kuingia uwanjani.
Wengi wa mashabiki hao walikuwa wakilalamika kufika uwanjani zaidi ya saa moja kabla ya mechi lakini walizuiwa kuingia na tayari kuna madai kwamba mabosi wa Liverpool wanataka suala hilo lichunguzwe ikiwamo kitendo cha mechi kuchelewa kuanza.