Na mwandishi wetu
Coastal Union Jumapili hii jioni wameitoa Azam katika Kombe la Shirikisho Azam kwa penalti 6-5 baada ya sare ya 0 -0 katika dakika 90 na 30 za nyongeza, timu hiyo sasa ina mitihani miwili mizito ukiwamo wa kujinasua na janga la kushuka daraja.
Kwa ushindi huo uliopatikana kwenye dimba la Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, Coastal sasa inasubiri kuumana na Yanga kumtafuta bingwa wa michuano hiyo ambaye ataiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa msimu wa 2022/23.
Baada ya ushindi huo Coastal sasa itakuwa imebakiwa na mitihani mikubwa miwili ya kushinda ili kujiweka salama, mtihani wa kwanza ni katika mechi zake za Ligi Kuu ya NBC Bara, timu hiyo hadi sasa imebakiwa na michezo minne na mtihani wa pili ni mechi yao ya fainali ya Kombe la Shirikisho Azam dhidi ya Yanga.
Kwanza Coastal inatakiwa ipambane kadri iwezavyo ili kuiangusha Yanga katika mechi hiyo ya fainali hasa kwa kuwa Yanga itakuwa haina cha kupoteza, hata ikifungwa nafasi yao ya kulibeba taji la Ligi Kuu ya NBC ni kubwa na hatimaye wataiwakilisha Tanzania kwenye michuano inayoandaliwa na CAF.
Yanga inahitaji pointi tatu tu ili ijitangaze bingwa wa Ligi Kuu, jambo ambalo halionekani kuwa gumu hasa kwa kuwa wapinzani wake wakuu wakiwamo Simba tayari wamekata tamaa ya kulitetea taji hilo na hivyo ubingwa kwa Yanga sasa ni suala la muda tu.
Mazingira ya aina hiyo, Coastal wanaweza kuyatumia vizuri ili kuibuka na ushindi hivyo kujihakikishia nafasi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika kwani vinginevyo watakuwa na kazi nyingine ngumu ya kupigania nafasi nne za juu ili walau kujiweka katika nafasi nzuri ya kuiwakilisha Tanzania Afrika.
Mtihani wa pili kwa timu hiyo ni kwenye Ligi Kuu ya NBC, hapo hapo wanakutana na Yanga kwa mara nyingine, hii nayo ni mechi muhimu kwao kushinda licha ya kwamba watakuwa ugenini na wanakutana na timu ambayo inahitaji pointi tatu ili itangaze ubingwa.
Baada ya hapo Coastal pia italazimika kushinda mechi zake tatu zilizobaki za ligi hiyo kwani kutofanya hivyo pia kutakuwa ni kujiweka katika janga la kushuka daraja, janga ambalo kwa sasa linaonekana liko mbali lakini katika hesabu za soka haliko mbali..
Timu hiyo kwa sasa ina pointi 34, maana yake ni kwamba ikishinda mechi zake zote zilizobaki itafikisha pointi 46 lakini ikipoteza mechi zilizobaki itabakiwa na pointi 34 ambazo zinaweza kufikiwa na timu za Prisons, Biashara na Mbeya Kwanza zilizo mkiani. Timu hizo zikishinda mechi zake zote zilizobaki zitafikisha pointi 36 na 39.
Iwapo Coastal itashinda mechi zote zilizobaki kwanza itakuwa imejitoa na mtego wa kushuka daraja lakini pia itakuwa imejiwekea akiba ya kuwa juu na hivyo kuwa na nafasi nzuri ya kuiwakilisha Tanzania katika michuano ya CAF itashindwa kuifunga Yanga kwenye mechi yao ya fainali lakini ikivurunda mechi zake za ligi na kuifunga Yanga maana yake ni kwamba Tanzania inaweza kujikuta ikiwakilishwa Afrika na timu iliyoshuka daraja.
Ni kweli kwamba Coastal anaweza kushinda baadhi ya mechi na kubaki kwenye ligi kutegemea matokeo ya mechi za timu nyingine lakini katika soka hesabu hizo si nzuri badala yake hesabu salama kwao ni kuhakikisha wanashinda mechi zao zote nne za ligi zilizobaki na pia kuhakikisha wanashinda mechi yao ya fainali ya Kombe la Shirikisho Azam dhidi ya Yanga.
Hiyo ndiyo hali halisi ambayo kocha wa Coastal, Juma Mgunda anatakiwa kuiangalia hasa baada ya ushindi dhidi ya Azam kwamba ana jukumu la kuhakikisha wachezaji wake hawabweteki.
Soka Coastal bado wana kazi ngumu
Coastal bado wana kazi ngumu
Related posts
Read also