Na mwandishi wetu
Ushindi wa mabao 2-0 ambao Yanga imeupata usiku huu dhidi ya Dodoma Jiji umeifanya timu hiyo kuendelea kujiimarisha kileleni katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC Bara.
Mabao hayo yaliyofungwa na Dickson Ambundo katika dakika ya 11 na Zawadi Mauya dakika ya 35 yameifanya timu hiyo kufikisha pointi 60 na hivyo kumuacha hasimu wake Simba kwa tofauti ya pointi 11 ingawa Simba inayoshika nafasi ya pili imecheza mechi 23 hadi sasa wakati Yanga leo imefikisha mechi yake ya 24.
Kwa upande mwingine ushindi dhidi ya Dodoma jiji si tu kwamba umeiimarisha Yanga kileleni lakini pia umeimarisha mbio za timu hiyo kuhakikisha inalitwaa taji hilo msimu huu hasa baada ya kuonekana kuyumba katika mechi tatu za hivi karibuni ambazo Yanga iliambulia matokeo ya sare ambayo yaliwakera mashabiki wa timu hiyo.
Sare dhidi ya Simba ilifuatiwa na sare nyingine mbili dhidi ya Ruvu Shootings na Tanzania Prisons, ziliibua hali ya wasiwasi kwa mashabiki wa timu hiyo kwenye mbio za kulisaka taji la ligi hiyo ambalo Simba imefanikiwa kulichukua mfululizo kwa misimu minne iliyopita na sasa inawania kuweka rekodi kwa kulibeba mara ya tano.
Kwa maana nyingine ushindi dhidi ya Dodoma ni kama vile umezika mzuka wa sare na sasa Yanga inaendelea na kasi yake ya kuhakikisha inakuwa bingwa msimu huu tena ikiwezekana bila kupoteza hata mechi moja.
Ushindi wa leo pia maana yake ni kwamba Yanga sasa inatakiwa kushinda mechi nne kati ya sita zilizobaki ili kutangazwa bingwa kabla ya ligi kumalizika, kwani ikishinda mechi hizo itakuwa imefikisha pointi 72 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote kwenye ligi hiyo.
Soka Yanga yajiimarisha kileleni
Yanga yajiimarisha kileleni
Related posts
Read also