Na mwandishi wetu
Fiston Mayele amedhihirisha ubora wake katika Ligi Kuu ya NBC akiwa na mabao 12 na hapana shaka ndiye mfungaji tegemeo wa Yanga.
Yote hayo kwa leo unaweza kuyaweka kando, habari kubwa ikawa ni je Mayele ataweza kuiadhibu Simba jioni ya leo kama ambavyo amekuwa akiziadhibu timu nyingine za ligi hiyo.
Amekuwa kwenye kasi ya ajabu katika mechi sita zilizopita, amefunga mfululizo huku Yanga ikiendelea kujiimarisha kileleni, ameziadhibu
KMC, Geita Gold, Mtibwa Sugar, Namungo, Kagera Sugar na Azam.
Rekodi hiyo tamu leo inaweza kuwekwa kando na swali linabaki je ataiua Simba na kuendeleza rekod hiyo?
Bao alilofunga dhidi ya Azam katika mechi iliyokuwa na ushindani mkali
limeendelea kuwa gumzo, ni bao tamu ambalo mashabiki wanazi wa Yanga wanaliita bao la ‘kideo’, nalo pia kwa leo linawekwa kando na hoja ya msingi inabaki pale pale kwamba je Mayele ataweza kuiadhibu Simba?
Nje ya mjadala wa Mayele kuiadhibu Simba kuna mjadala mwingine wa nani wa kumdhibiti Mayele, hapo wanatajwa zaidi mabeki wawili wapambanaji,
Joash Onyango na Enock Inonga.
Mabeki hawa katika mechi iliyopita walikuwa kama vile wamepangiana na kupokezana majukumu ya kuhakikisha Mayele hatetemi, ukimkosa Inonga
utamkuta Onyango, ingawa ni Onyango aliyeonekana zaidi katika matukio kadhaa akimdhibiti Mayele.
Katika dakika ya 20 ya mchezo huo, Mayele alipenyezewa pasi na kushindana kwa kasi na Onyango kwa kila mmojawao kutaka kuuwahi mpira,
wakati ikiaminika hiyo ilikuwa nafasi ya Mayele kuiadhibu Simba mapema, Onyango alimzidi kwa kasi kidogo na kuondoa hatari.
Dakika nne baadaye, Mayele aliunasa mpira na kuupenyeza katikati ya miguu ya Onyango, wakati Mayele akikimbia kwa kasi kuuwahi mpira huo
ili kuiadhibu Simba, alichofanya Onyango ni kumzuia Mayele kwenye njia, tukio hilo lilimfanya Onyango apewe kadi ya njano na Yanga
kupewa mpira wa adhabu.
Mayele na Onyango walikutana katika tukio jingine katika dakika ya 33, safari hii wakishindania mpira wa juu, alichofanya Onyango ni kumpa
mwili Mayele, alitumia bega kumtoa kwenye mstari na hivyo kumfanya ashindwe kuutumia mpira huo kuifunga Simba.
Dakika mbili kabla ya mapumziko, Mayele aliunganishiwa mpira wa juu
ambao kipa wa Simba, Aishi Manula alidhamiria kuudaka lakini hesabu
zilikataa baada ya kuteleza jambo lililompa Mayele nafasi ya kuuwahi mpira huo huku Onyango akimfukuzia lakini akiwa ameudhibiti mpira
vizuri Mayele naye akataleza na kumrahisishia Onyango kazi ya kuondo hatari langoni mwake.
Ukimuweka kando Onyango, Inonga naye mara kwa mara alikuwa karibu na mchezaji huyo pale ambapo Onyango alikosekana, na hadi wakati Mayele
anatolewa katika dakika ya 83, ni Inonga aliyemsindikiza kwenda kwenye
benchi.
Inonga, beki mwingine kisiki wa Simba alikuwa akihaha kila kona kuhakikisha Simba haifungwi hapo hapo ni kama alijipa kazi nyingine ya kumdhibiti Mayele asiteteme.
Matukio yote hayo yanabaki kuwa tisa, je leo nani kati yao atakayehakikisha Mayele hafanyi yake na je Mayele ataitumia Simba kuendeleza rekodi yake ya mabao mfululizo? Yanga hadi sasa inaongoza ligi ikiwa imekusanya pointi 54 katikamichezo 20 wakati Simba ina pointi 41 ikiwa imecheza michezo 19.