New Delhi, India
Filamu ya Andhaa Kaanoon iliyotoka mara ya kwanza mwaka 1982 imeendelea kubebwa na maudhui yake yenye ujumbe wa haki katika jamii.
Katika filamu hiyo, Amitabh Bachchan, staa wa zama hizo, ameubeba vyema uhusika hasa namna ambavyo filamu hiyo inadhihirisha hoja kwamba duniani kuna sheria lakini sheria si kila wakati inasimamia haki.
Amitabh ambaye ameshiriki filamu hiyo kwa jina la Khan, anabambikiwa kesi ya mauaji akidaiwa kumuua Gupta (Amrish Puri) na kujikuta akihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela, mkewe anabakwa na mwishowe anaamua kujiua pamoja na mtoto wao wa pekee, Neelu.
Baadaye Amitabh anabaini kwamba Gupta hakufa na yeye hakutendewa haki, alihukumiwa kimakosa hivyo anaamua kulipiza kisasi kwa kumuua Gupta.
Wakati ikiwa imepita miaka takriban 38 tangu Amitabh ashiriki katika Andhaa Kaanoon, mkongwe huyu ambaye filamu zake miaka ya 1980 na 1990 mwanzoni zilikuwa kimbilio la wapenzi wa filamu nchini, kwa sasa anaendelea kusumbua katika filamu wakati badhi ya wenzake wa zama hizo wakistaafu na wengine kutangulia mbele ya haki.
Kwa mpenzi yeyote wa filamu wa miaka ya 1980 hasa filamu za India ukimtajia jina la Amitabh utamrudisha katika filamu za zama hizo kuanzia Deewaar na Sholay zinazotajwa kumpaisha na kumfanya aanze kuwa staa kuanzia miaka ya 1970 mwishoni na 1980 mwanzoni.

Mwaka 1999, Sholay ilitajwa na BBC India kuwa ni Filamu ya Milenia na pamoja na Deewar zote pia katika kipindi hicho hicho zilichaguliwa na Indiatimes Movies kwenye orodha ya filamu bora 25 za Bollywood.
Jina la Amitabh liliendelea kuwa juu nchi mbalimbali duniani hasa aliposhiriki vizuri filamu za Kasme Vaade, Muqaddar Ka Sikandar, Ganga Ki Saugandh, Don, Besharam na Trishul, filamu hizi ni kama vile zilidhihirisha uwezo wake na kumfungulia zaidi njia za mafanikio.
Pia alianza kufurahia ubora wa kazi zake kwa kuvuna fedha nyingi zaidi na kupata tuzo kupitia filamu ya Suhaag pamoja na Mr Natwarlal, Kaala Patthar, The Great Gambler na Manzil kabla ya kumshirikisha mkewe Jaya katika filamu ya Silsila.
Hiyo ilikuwa kama chachu ya mafanikio, aliendelea kuonyesha ubora wake huku akilishika kisawasawa soko la filamu kwa ushiriki wake katika filamu za Shaan, Ram Balram, Naseeb, Lawaaris, Kaalia pamoja na Shakti.
NI katika kipindi hicho hicho wakati jina likiwa juu, ndipo alipozidi kukonga nyoyo za mashabiki kwa filamu ya Andhaa Kaanoon ambayo maudhui yake yameendelea kuwa tukio la kipekee kwa kizazi hadi kizazi na waliobahatika kuiona miaka hiyo baadhi yao hawakutosheka kuiona mara moja, kumbi za sinema za Avalon, Empire, New Chox na kwingineko jijini Dar es Salaam zilifurika mashabiki kama ilivyokuwa kwa Metropole na Elite jijini Arusha na kwingineko Tanzania.
Mwaka 1984, Amitabh alijiingiza kwenye siasa na kusimama katika filamu hadi 1987 aliporudi tena kwa muda mfupi kabla ya kutangaza kustaafu mwaka 1992 wakati huo akiwa na miaka 50.
Wakati ikitarajiwa kwamba huo ulikuwa mwisho wa zama za Amitabh, hali ikawa tofauti aliendelea kushiriki filamu na kutokana na nguvu alizonazo anaendelea kukimbiza Bollywood hata katika zama hizi za kidigitali.
Ni mwaka 2018 tu, Amitabh akiwa na miaka 76 ameshiriki filamu kadhaa ikiwamo ile ya Thugs Of Hindostan akiwashirikisha kina Aamir Khan, Fatima Shaikh na Katrina Kaif.
Kwa wanaofuatilia filamu kwenye Zee World bila shaka Amitabh si mgeni kwao mara kadhaa amekuwa akionekana katika filamu zake za zamani na hizi za zama za kidigitali, lakini swali ni je ataendelea hata akiwa na miaka 80 au atatangaza kustaafu rasmi.